Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf, katika khutba za Swala ya Ijumaa alizozitoa katika Husainiya A’dham Fatimiya, Najaf Ashraf, alisema: Huku ngoma za vita zikipigwa na kauli za vitisho zikienea kila upande katika anga ya eneo, Trump ameipa Iran muda wa siku 15. Kwa upande mwingine, Iran imefunga Mlango wa Hormuz, imefanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Urusi katika eneo, na imetuma ujumbe kwa Umoja wa Mataifa kwamba uvamizi wowote dhidi yake utamaanisha haki ya kujibu kisheria dhidi ya kambi zote za Marekani.
Aliongeza kuwa: Kwa vyovyote vile si kwa manufaa ya yeyote kwamba eneo liwake moto; Iran ni mpiganaji shupavu na ina uwezo wa kubadilisha kanuni za mchezo. Dunia haipaswi kusahau mkono wa ghaibu uliosaidia huko Tabas na kuziangusha ndege za Marekani bila uingiliaji wa kibinadamu.
Katika mhimili wa kimataifa
Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf aliendelea kwa kuashiria kufanyika kwa “Baraza la Amani” akisema: Baraza hili limeundwa Washington chini ya usimamizi wa Marekani. Nchi tano za Kiarabu za mwambao wa Ghuba zimelichangia dola bilioni tano, lakini hata sehemu ya kumi ya kiasi hicho haijatengwa kwa ajili ya Ghaza. Tunaamini kuwa baraza hili kimsingi ni chombo cha kulazimisha ulezi na utawala juu ya dunia na kufuta nafasi ya Umoja wa Mataifa.
Katika mhimili wa ndani
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, huku akirejea ripoti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq, alisema: Ndani ya nchi, visa vya ukatili wa kifamilia vimeongezeka kwa asilimia 150. Kwa mujibu wa takwimu rasmi: ukatili wa mume dhidi ya mke visa 19,000; ukatili wa mke dhidi ya mume visa 5,000; ukatili wa baba dhidi ya watoto visa 1,000; ukatili wa watoto dhidi ya baba visa 3,000; na ukatili kati ya ndugu visa 1,000. Hivyo, kwa mara ya kwanza takwimu za ukatili wa kifamilia nchini zimeongezeka kwa zaidi ya mara moja na nusu.
Aliongeza: Katika suala hili, inahitajika tiba ya kitamaduni, vyombo vya habari na kisheria, na mizizi ya jambo hili kama vile madawa ya kulevya, maudhui machafu katika mitandao ya kijamii na ukosefu wa ajira, iondolewe kabisa.
Kuhusu vyombo vya habari na kazi za kisanii
Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf, akiyakosoa baadhi ya vipindi vya televisheni, alisema: Katika baadhi ya vituo vya Iraq, kuna misururu ya tamthilia zinayorushwa katika mwezi wa Ramadhani zinayovunja heshima na haiba ya jamii. Wizara husika pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu zinapaswa kubeba jukumu la kuzuia kurushwa kwa vipindi vya aina hii.
Katika sehemu nyingine ya khutba yake alisema: Mji wa Najaf Ashraf umechukua nafasi ya kwanza nchini Iraq katika kupambana na misimamo mikali. Aidha, mji huu umeshuhudia miradi mikubwa ya huduma katika uwanja wa uwekaji lami na usafi wa mji, ujenzi wa madaraja, kuhudumia maeneo duni na kutatua tatizo la uvamizi na ukiukwaji wa ujenzi. Tunapaswa kuushukuru uongozi wa kiraia wa Najaf Ashraf kwa hili na kuwapongeza watu wema katika mji huu.
Khutba ya kidini
Khatibu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf katika khutba ya kidini alizungumzia tafsiri ya kiroho ya mwezi wa Ramadhani na kusema: Ni nini hutokea katika mwezi wa Ramadhani? Kinachotokea ni mabadiliko ya kiulimwengu, kama alivyosema Mtume Mtukufu (s.a.w.w) katika khutba yake:
«أَنْفَاسُكُمْ فِيهِ تَسْبِيحٌ، وَنَوْمُكُمْ فِيهِ عِبَادَةٌ، وَعَمَلُكُمْ فِيهِ مَقْبُولٌ، وَدُعَاؤُكُمْ فِيهِ مُسْتَجَابٌ، فَمَنْ حَسَّنَ مِنْكُمْ خُلُقَهُ فِي هَذَا الشَّهْرِ كَانَ لَهُ جَوَازٌ عَلَى الصِّرَاطِ، يَوْمَ تَزِلُّ فِيهِ الْأَقْدَامُ، وَأَبْوَابُ الْجِنَانِ فِيهِ مُفَتَّحَةٌ، وَأَبْوَابُ النِّيرَانِ فِيهِ مُغَلَّقَةٌ»
“Pumzi zenu katika mwezi huu ni tasbihi, usingizi wenu ni ibada, amali zenu zinakubaliwa na dua zenu zinajibiwa. Yeyote miongoni mwenu atakayeboresha tabia yake katika mwezi huu atakuwa na ruhusa ya kupita juu ya Sirat siku ambayo miguu itateleza; na milango ya Pepo katika mwezi huu imefunguliwa, na milango ya Moto imefungwa.”
Aliendelea kusema: Haya si maneno ya kuhamasisha tu, bali ni mabadiliko halisi katika mfumo wa uumbaji. Miongoni mwa mabadiliko makubwa zaidi ni kushuka Qur’ani Tukufu kutoka mbinguni hadi ardhini na uhusiano wa moja kwa moja kati ya mbingu na moyo wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w). Hii ina maana kwamba, katika mwezi huu mtukufu kuna uhusiano hai kati ya mbingu na ardhi. Lakini swali ni hili: Mbele ya mabadiliko haya ya Kiungu, nini kinachotakiwa kutoka kwetu?
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji alieleza kwamba; Mtume Mtukufu (s.a.w.w) anajibu kwa kusema:
«إِنَّ ظُهُورَكُمْ ثَقِيلَةٌ بِأَوْزَارِكُمْ فَخَفِّفُوا عَنْهَا بِطُولِ سُجُودِكُمْ، وَإِنَّ أَنْفُسَكُمْ مَرْهُونَةٌ بِأَعْمَالِكُمْ فَفُكُّوهَا بِكَثْرَةِ اسْتِغْفَارِكُمْ»
“Hakika migongo yenu imekuwa mizito kwa sababu ya dhambi zenu; basi ifanyeni iwe nyepesi kwa kurefusha sijda zenu. Na hakika nafsi zenu zimefungwa kwa sababu ya matendo yenu; basi zifungueni kwa wingi wa kuomba msamaha.”
Maoni yako